Pages

Friday, June 6, 2014

makala PALIPO NA RUSHWA HAKUNA MAENDELEO



Na; JAME JOVIN
Kibondo Kigoma
Ndugu zangu wasomaji wa Makala hii ni vema kabla ya kuendelea niwakumbushe kidogo misemo na methali za wahenga. Kuna methali nyingi zenye mafunzo zilizotungwa na mababu zetu hapo zamani ama wahenga, mojawapo ya methali hizo ni “umoja ni nguvu utengano ni udhaifu” na wengine walisema kuwa “kidole kimoja hakivunji chawa”. Ndugu zangu palipo na rushwa siku zote hakuna maendeleo na sisi wananchi ndio walengwa wa hayo maendeleo, tusiposhiriki kutokomeza rushwa ni dhahili kuwa tutaendelea kupewa misemo ya aina mbali mbali na wenzetu kama “there is no hurry  in Africa” wakimaanisha afrika hakuna haraka au “Africa is a dark place” yaani afrika ni bara la giza na hayo maendeleo yatabaki kuwa ni ndoto kutokana na sisi wenyewe kutopenda kushiriki shughuli za maendeleo, kama kutokomeza rushwa. Methali hizi nilizoanza nazo kuzitamka utaona umuhimu wake kadri utakavyoendelea kusoma Makala hii.
Kibondo ni kati ya wilaya ya chache Tanzania  zilizojaliwa mali asili za kutosha na za kila aina. Mfano Ardhi yenye rutuba, Hali nzuri ya hewa,Mito yenye Samaki, Wanyama Pori na Milima ya aina mbali mbali ambavyo hivyo vyote ni vivutio vya Watalii ambavyo kama vingetumika vema Taifa lingejipatia pato la kutosha kuendeleza shughuli za kiserikali pamoja na jamii kwa ujumla. Lakini kwetu sisi ni tofauti, tuna matatizo mengi hata zaidi ya wilaya  ambazo hawana kitu chochote, na tatizo kubwa linaloikabiri Kibondo ni watu wengi hususani vijana kutopenda kujishughulisha ama kushiriki katika shughuli za maendeleo. Wengi wetu hata tukiona kwa macho mtu anatoa ama kupokea rushwa tunadhani kuwa hayatuhusu hivyo hata kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji tunashindwa.
Ndugu zangu elimu ni jambo la msingi sana katika harakati za maendeleo haiwezekani jamii ishuhudie utoaji na upokeaji wa rushwa halafu ishindwe kutoa ushirikiano kwa maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa kwa madai kuwa hayawahusu. Tutaangamia kwa kudhani hayatuhusu na kwa kudhani hayatuhusu rasrimali zetu ndivyo zinavyoondoka na sisi kubaki masikini. Hebu jifikirie jengo la shule kijijini kwako linajengwa chini ya kiwango na wewe ulishiriki kama kibarua lakini kutoa taarifa kwa vyombo kama TAKUKURU ili waje wazuie unashindwa hatimaye pesa inaliwa kisha baada ya miaka mitano mwanao anakosa mahali pa kusomea. Unadhani mwenye hasara ni nani ?. Je ni yule aliyepewa kandarasi ya kujenga darasa kisha akalijenga chini ya kiwango au ni wewe ambaye hukutaka kutoa ushirikiano kwa vyombo husika hususani Takukuru.
Jamii nzima tunayo majukumu ya kuhakikisha tunapambana na rushwa kwa njia yoyote ile. Njia ya kwanza ni kuhakikisha hatupokei wala kutoa rushwa hii itasaidia sana katika kupunguza tatizo hili hebu fikiria unataka huduma katika zahanati ya kijiji, mkeo anataka kujifungua ni saa mbili za usiku muuguzi au mganga ameshalala lakini cha ajabu anakataa kutoa huduma mpaka amepewe shilingi elfu 10 bila aibu unatoa pesa ile, mkeo anajifungua halafu unashindwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama. Je, itakuwaje kwa mtu ambaye hana hiyo elfu 10? kumbuka kuwa palipo na rushwa siku zote hakuna maendeleo.
Ndugu msomaji Rushwa ni mbaya iwe kutoa ama kupokea kwa mtu mmoja mmoja na pia kwa jamii. Rushwa husababisha maangamizi na hasara kwa umma, huharibu na kupoteza ndoto za maendeleo ya wanajamii, Rushwa huleta udanganyifu na  uongo mahala pa uaminifu, dhuluma mahala pa haki, na hofu mahala pa amani na utulivu.

Palipo na rushwa siku zote hakuna maendeleo mathalani ajira zinajitokeza hususani za kwenda kujitolea JKT pale Kanembwa au wanahitajika maafisa watendaji katika kata zetu labda za Kitahana , Kumsenga ama Bunyambo ama katika mashirika binafsi kuna nafasi kama kumi (10) za kazi kwa bahati mbaya bila kutoa kitu kidogo hata kwenye usaili huitwi. Sio watu wote wenye uwezo wa kununua kazi, wakati mwingine mazingira yanatatanisha mno. Mathalani, utakuta kijana ana vigezo vyote vya kazi, ila kwa vile hana uwezo wa kutoa kitu kidogo, na kwa bahati mbaya masikini huyu hamjui mtu pale anapo omba ajira basi hana chake tena, na kama tujuavyo sote kuwa rushwa ni adui wa haki, kwa hiyo anakuwa amepoteza haki yake ya msingi na kwa bahati mbaya kijana huyu anashindwa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TAKUKURU ili kushughulikia unyama huo ili mwisho wa siku rushwa ikomeshwe kama sio kumalizwa kabisa.

Askari wa usalama bara barani kila siku wanapokea rushwa kutoka kwa madereva boda boda ama madereva wa magari ya abiria cha kushangaza hakuna hata anayetoa taarifa ama kulalamika popote, matokeo yake kipato chake kisichozidi shilingi elfu 20 kila siku anakigawana na askari hao bila kujua kuwa anapoteza mapato ya serikali ambayo yangeingia kama ushuru ama faini halali na  baadae yangerudi na kuinufaisha jamii kwa ujumla katika maswala ya bara bara , zahanati ama maji safi.

Ndugu zangu nataka mjue kuwa aneyetoa na anayepokea rushwa wote wana makosa na wanapaswa kuadhibiwa. Kila utakapoona dalili za rushwa ni vema ukatoa taarifa kwa vyombo husika ili kuweka mazingira ya kumkamata mtuhumiwa na wewe kama Mtanzania utakuwa umeonesha uzalendo wako kwa Taifa na kuokoa mali ambayo ingepotea bila kufanya kazi yoyote ya maendeleo kwa Taifa lako.

Ndugu msomaji lazima uchukue nafasi yako katika mambo ya nchi usimwachie tu mtendaji ama mtumishi bila ushiriki wako. Hakuna kitakachowezekana bila ya  kutimiza wajibu wako na kubaki tu kuwa mtazamaji na mwisho wa siku utageuka kuwa mlalamikaji. Kama kiongozi wako wa kijiji anapokea rushwa kwa nini ukae kimya usitoe taarifa kwa Takukuru? na mwisho wa siku hatua ichukuliwe na maendeleo ya kijiji na jamii kwa ujumla yaonekane.
Ni wakati wa kila mwana Kibondo kwa imani yake kuwa na hofu ya Mungu kwa  kuwa mtu anayemjua Mungu na mwenye hofu ya Mungu hawezi kufanya mambo maovu ambayo yanamchukiza Mungu na yanaichukiza jamii.
“Mcha Mungu wa kweli atatenda haki; hawezi kumdhulumu binadamu mwenzake, hawezi kudai rushwa ili atoe huduma kwa mtu, hawezi kuiba fedha za umma wala kujihusisha na  ufisadi wa aina yoyote au uonevu wa aina yoyote kwa maana anajua hayo yote ni dhambi mbele za Mungu

Nadhani sasa ndugu msomaji utakuwa umeshaelewa ni kwa nini nimeanza na zile methali pale mwanzo wa Makala hii na zaidi nilikuwa nalenga kuwa haiwezekani maafisa wa TAKUKURU wakafanya kazi hii bila ushiriki wako kwa namna moja ama nyingine la sivyo tutabaki kuwalaumu. Kama mzalendo ni lazima ushirikiane na maafisa hawa katika kutokomeza rushwa miongoni mwa jamii. Pale unapohitajika basi utoe ushirikiano bila kusita wengi wetu tunapoitwa mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi huwa tunakimbia hivyo kesi nyingi kuishia kufutwa mahakamani kwa kukosa ushahidi na kusababisha kazi hii iwe ngumu kweli kweli kwa TAKUKURU na mwisho wa siku jamii hupoteza kabisa Imani na chombo hiki chenye majukumu mazito ya kuhakikisha rushwa inabaki kuwa historia hapa nchini. Ndugu msomaji  kumbuka kuwa palipo na rushwa hakuna maendeleo siku zote  hivyo unapaswa kushiriki kadri uwezavyo kama mzalendo katika kuitokomeza.
Mwisho kabisa ni vema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) iongeze juhudi za kuhakikisha wanatembelea vijiji vyote na kutoa elimu kwa wananchi mara kwa mara ili kuwaelewesha wananchi namna ya kushiriki katika mapambano haya ambayo mwisho wa siku kama elimu itaeleweka basi rushwa itakoma au kupungua miongoni mwa jamii. Tukifanikiwa katika mapambano haya, rushwa ya ngono, ajira kwa wasiositahili, ujenzi ya majengo ya umma chini ya kiwango  na mengine mengi vitakoma kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. MWISHO      0786614043

No comments:

Post a Comment