Fidelis Butahe, Mwananchi
Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ameeleza namna alivyoibua
sakata la uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow na
kudokeza kuwa kitendo cha baadhi ya watuhumiwa kugoma kujiuzulu,
kinaonyesha kuna watu zaidi wanahusika.
Kafulila
(32), ambaye alikuwa akiulizia suala hilo kila mara bungeni hadi uamuzi
wa kulijadili ulipofikiwa, amesema ataendelea kulifuatilia hadi aone
mwisho wake.
Akaunti
hiyo ilifunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhifadhi fedha za malipo
ya tozo ya ufuaji umeme baada ya Tanesco kuingia kwenye mgogoro na
Kampuni ya IPTL na suala hilo kupelekwa mahakamani.
Kwa
mujibu wa masharti ya uendeshaji wa akaunti za escrow, fedha hizo
zilitakiwa zitolewe baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa mgogoro huo,
lakini wakati ilitaka pande hizo mbili zikutane na kukokotoa viwango vya
tozo hizo, fedha hizo zilitolewa na kulipwa kwa mmiliki mpya wa Kampuni
ya Pan African Power Solutions (PAP), jambo lililosababisha kuibuka kwa
kashfa hiyo.
Akizungumza
kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Kafulila alisema
alilinasa suala hilo kwenye vyombo vya habari na baadaye kupewa kurasa
nne za maelezo ya sakata hilo, lakini baada ya kuliingiza kwenye chombo
hicho cha kutunga sheria, wabunge wenzake waliendelea kumwongezea
nyaraka hadi zikafikia kurasa 604.(P.T)
"Lilikuwa
ni jambo la furaha kwangu kuona kwamba wabunge wenzangu wamenipa
nyaraka nyingi pamoja na kwamba walishakuwa nazo awali, lakini hawakuwa
wametaka kuzitoa hadi nilipoingiza suala hili bungeni," alisema Kafulila
ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2010... "Nyaraka hizi
zilinisaidia sana."
Kupata
ufahamu wa suala hilo kulikuwa kama bahati kwa mbunge huyo. "Nilianza
kulifahamu suala la escrow nikiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere wakati nikienda Uswisi. Lilikuwa limeandikwa katika gazeti
(jina tunalo) ambalo katika ukurasa wake wa kwanza walikuwa wamechora
skendo mbalimbali za IPTL, kuanzia mwaka 1995 hadi 2014," alisema.
Aliongeza
kuwa alipotoka safari aliikuta habari hiyo ikiwa imeandikwa kwa kina
katika gazeti The Citizen na hivyo kumfanya ajenge hamu ya kutaka kujua
undani wake. Alisema alianza kulifuatilia suala hilo kwa kuwasiliana na
mmoja wa mawaziri wa Wizara ya Nishati na Madini ambaye awali alikuwa na
utaratibu wa kumjulisha kila jambo linalofanywa na wizara hiyo.
"Nilimweleza
mambo ambayo wizara inatakiwa kuyajibu kuhusu wizi wa fedha hizo ambao
unaandikwa katika magazeti. Alinijibu kuwa wanaoandika habari hizo ni
wababaishaji na wanaandika vitu wasivyovijua," alisema.
Alisema
kutokana na unyeti wa suala hilo na sifa walizokuwa wakipewa watendaji
wa Wizara ya Nishati na Madini, hakukata tamaa na kuamua kulipeleka
suala hilo bungeni ili litolewe ufafanuzi wa kina.
"Kabla ya
mkutano wa Bunge kuanza nilimtafuta mtu mmoja (anamtaja jina) ambaye
alinipa kurasa nne tu kuhusu IPTL na escrow tena kwa siri kubwa.
Nilipozisoma nilielewa suala hilo. Mei mwaka huu wakati nikichangia
hotuba ya Waziri Mkuu bungeni niliibua sakata hilo na kutaja majina ya
wahusika," alisema.
endelea na stor hii kwa kubonyeza hapa
No comments:
Post a Comment