Pages

Saturday, March 8, 2014

bunge la katiba ngumi mkononi







Ngumi
mkononi ndilo neno jepesi ambalo linafaa kutumika baada ya vurugu kubwa
kutokea jana ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi cha
kumlazimisha Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina
kabla ya wakati wake.



Semina ya wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba, imekuwa ikianza saa 4:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana kabla ya
kuendelea tena kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 3:00 usiku. Jana, katika
kipindi cha asubuhi, semina hiyo iliahirishwa saa 6:17 licha ya kuanza
saa tano asubuhi kabla ya kurejea tena saa 10 jioni.



Ngumi zilitaka kupigwa baada ya Waziri
wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakari Hamis Bakari kuhoji uhalali
wa Christopher Ole Sendeka na Ummy Mwalimu kuchangia wakati hawakuwamo
katika orodha ya wachangiaji jambo ambalo liliibua mjadala mkali na
kurushiana maneno kabla ya Mwenyekiti Pandu Ameir Kificho kuahirisha
semina hiyo.








Chanzo cha vurugu


Kificho alimpa Ole Sendeka nafasi ya
kuchangia Kifungu namba 58 cha rasimu ya kanuni na baada ya kutoa
mchango wake, Hamisi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kanuni, alisimama
na kumtaka Mwenyekiti Kificho kuacha kuwateua watu ambao hawamo katika
orodha ya wachangiaji.



Kificho hakumsikiliza na badala yake,
alimpa nafasi mjumbe mwingine wa Bunge hilo Ummy Mwalimu ambaye pia ni
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuchangia. Hata hivyo kabla
hajafanya hivyo, Bakari alisimama tena na kumzuia kuchangia kwa madai
kuwa hakuwamo kwenye orodha ya wachangiaji.



"Mheshimiwa Mwenyekiti, kama
tutaendelea na utaratibu huu suala la kuchangia kanuni linaweza
kutupeleka hadi miezi sita bila ya kumaliza. Haya majina hayakuwemo
kwenye orodha ya wachangiaji na huyo aliyemaliza sasa Ole Sendeka, naye
hakuwamo, naomba tuache mchezo huu," alisema Bakari.



Aliendelea: "Sekretarieti
inakuchomekea majina mwenyekiti na kama hivyo ndivyo, basi tunatakiwa
kuwachukulia hatua kali hawa kwani tunataka kujadili hoja ambazo
hazimo."



Bakari alisema wajumbe waliotakiwa
kuchangia ni wale ambao walipeleka majina kwa makatibu wa Bunge hilo
pamoja na michango yao kwa maandishi ili wapewe nafasi ya kuzungumza,
lakini Kificho alikuwa akiwateua wajumbe ambao hawamo katika orodha
hiyo.



Kificho ajibu


"Mimi sina tatizo na jambo hilo,
mkisema tuendelee basi sawa, lakini mkitaka tufanye mambo kwa uzuri
inawezekana pia, jambo la muhimu ni kuwa tupo hapa kutengeneza Katiba ya
wananchi siyo ya vyama."



Kelele zilianza kusikika huku wajumbe
wakiimba kuwa mwenyekiti anayumba... na kumtaka mwenyekiti atoke nje na
kukiacha kiti, kwani anafanya upendeleo.



 Kelele hizo ziliambatana na wajumbe
hao kuwasha vipaza sauti bila utaratibu. Mjumbe Sadifa Juma Khamis ndiye
aliyekuwa wa kwanza kuwasha kipaza sauti chake na kusimama wakati wote
akisema anataka kuchangia, huku akiungwa mkono na wajumbe wengine
kadhaa.



Kutokana na tukio hilo, Kificho
alilazimika kumwita Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu
ambaye alikiri kuwa yako majina ambayo hayakuwamo kwenye orodha, lakini
kwa mwenyekiti yalionekana.



Moto zaidi uliwaka baada ya Ole
Sendeka kusimama hata bila ya kupewa nafasi na kusema anazijua kanuni
vizuri na kwamba asingeweza kuzivunja.



"Nilijua hayo yote na mimi siyo dhaifu
wa kanuni kwani najua kila kitu na tulikwenda tangu mwanzo; mimi,
Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Peter Serukamba, ndiyo maana majina yetu yamo
humo ila kama mapigo yetu yanawakwaza wengine waseme, siyo jukumu la
mimi kupeleka mapendekezo yangu kwa Bakari, labda kama wewe una msimamo
wako na chama chako," alisema Ole Sendeka.



Kauli hiyo ilizusha kelele za wajumbe
ndani ya ukumbi, huku Kificho akiwatuliza na kusema Ole Sendeka
aliteleza ulimi na kumtaka aombe radhi kama anataka, lakini mjumbe huyo
aligoma kwa kuonyesha ishara ya mikono, jambo ambalo lilimfanya Bakari
kusimama tena.



Bakari alisimama na kueleza uzoefu wake wa miaka 34 kwenye Bunge akijisifu kuwa yeye ni zaidi ya Ole Sendeka.


"Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sihitaji
kuombwa msamaha na Ole Sendeka, nimekuwa kwenye mabunge haya tangu mwaka
1980, leo hii mtu kutoka Simanjiro miaka 10 iliyopita hawezi
kunitisha," alisema Bakari.



Wengine nusura wapigane


Kauli hiyo iliwafanya wajumbe wengi
bungeni kusimama, huku wengine wakitaka kupigana ngumi baadhi wakisema:
"Twende nje tukapigane, twende nje tukapigane..."



Waliokuwa wakibishana zaidi ni Abdalla
Sharia ambaye alitaka kupigana na Khatibu Haji kabla ya kuzuiwa na
wenzao, huku Tauhida Nyimbo akitaka kuzikunja na Seleman Bungara
(Bwege).



Wakati Bunge likiwa limechafuka na
kukiwa na kelele nyingi, mwandishi wa habari hizi alimuona, Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda akimuonyesha kwa ishara ya
mikono Kificho kuahirisha semina.



"Naahirisha semina hii mpaka saa kumi
jioni," alisema Kificho na kuwafanya wajumbe kupiga kelele huku wengine
wakishangilia na baadhi wakiguna.



Nje ya ukumbi


Wakiwa nje ya ukumbi, Ole Sendeka
alisema hoja zake ni nzito na haziwezi kuzimwa na Bakari ambaye
anaonekana kuwa na masilahi binafsi.



Alisema yeye pamoja na wenzake (Ummy
na Serukamba), bado wanatarajia kuwasha moto kwa kila kifungu ili mambo
yaweze kukaa vizuri na kuwa kilichotokea kwake ni burudani.



Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema tatizo kubwa lililosababisha mambo hayo ni misimamo ya
mwenyekiti kuyumba wakati wote.



Hata hivyo, alilaani kitendo cha
wajumbe wengine kuwa na hoja alizoziita za kitoto kwa kuzomeazomea
akisema hata kama kiti kinayumba, bado walipaswa kuwa watulivu na
kuangalia kilichowapeleka Dodoma.



Mjumbe mwingine, Charles Tzeba ambaye
pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, alitetea kauli ya Sendeka na kusema
hata kama hakuwa kwenye orodha alipaswa kuchangia kwani hiyo ilikuwa ni
semina ambayo kila mtu anayo haki ya kuchangia wakati wowote.



Bunge liliporejea jioni, wajumbe
wawili-James Mbatia na Profesa Mark Mwandosya walisimama na kutoa nasaha
za kutuliza jazba pale wajumbe wanapokwaruzana, huku Mwenyekiti Kificho
akisema kilichotokea asubuhi kilitokana na yeye kutokujua kwamba baadhi
ya wajumbe hawakuwa katika orodha.(P.T)



Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment