Na; JAME JOVIN
Kibondo Kigoma
Ndugu zangu wasomaji wa Makala hii ni vema kabla
ya kuendelea niwakumbushe kidogo misemo na methali za wahenga. Kuna methali
nyingi zenye mafunzo zilizotungwa na mababu zetu hapo zamani ama wahenga,
mojawapo ya methali hizo ni “umoja ni nguvu utengano ni udhaifu” na wengine walisema
kuwa “kidole kimoja hakivunji chawa”. Ndugu zangu palipo na rushwa siku zote hakuna maendeleo na sisi wananchi ndio
walengwa wa hayo maendeleo, tusiposhiriki kutokomeza rushwa ni dhahili kuwa
tutaendelea kupewa misemo ya aina mbali mbali na wenzetu kama “there is no hurry in Africa” wakimaanisha afrika hakuna haraka
au “Africa is a dark place” yaani afrika ni bara la giza na hayo maendeleo
yatabaki kuwa ni ndoto kutokana na sisi wenyewe kutopenda kushiriki shughuli za
maendeleo, kama kutokomeza rushwa. Methali hizi nilizoanza nazo kuzitamka
utaona umuhimu wake kadri utakavyoendelea kusoma Makala hii.
Kibondo ni kati ya wilaya ya chache Tanzania zilizojaliwa mali asili za kutosha na za kila
aina. Mfano Ardhi yenye rutuba, Hali nzuri ya hewa,Mito yenye Samaki, Wanyama
Pori na Milima ya aina mbali mbali ambavyo hivyo vyote ni vivutio vya Watalii
ambavyo kama vingetumika vema Taifa lingejipatia pato la kutosha kuendeleza
shughuli za kiserikali pamoja na jamii kwa ujumla. Lakini kwetu sisi ni
tofauti, tuna matatizo mengi hata zaidi ya wilaya ambazo hawana kitu chochote, na tatizo kubwa
linaloikabiri Kibondo ni watu wengi hususani vijana kutopenda kujishughulisha
ama kushiriki katika shughuli za maendeleo. Wengi wetu hata tukiona kwa macho
mtu anatoa ama kupokea rushwa tunadhani kuwa hayatuhusu hivyo hata kutoa
taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji tunashindwa.
Ndugu zangu elimu ni jambo la msingi sana katika
harakati za maendeleo haiwezekani jamii ishuhudie utoaji na upokeaji wa rushwa
halafu ishindwe kutoa ushirikiano kwa maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa kwa madai kuwa hayawahusu. Tutaangamia
kwa kudhani hayatuhusu na kwa kudhani hayatuhusu rasrimali zetu ndivyo
zinavyoondoka na sisi kubaki masikini. Hebu jifikirie jengo la shule kijijini
kwako linajengwa chini ya kiwango na wewe ulishiriki kama kibarua lakini kutoa
taarifa kwa vyombo kama TAKUKURU ili waje wazuie unashindwa hatimaye pesa
inaliwa kisha baada ya miaka mitano mwanao anakosa mahali pa kusomea. Unadhani
mwenye hasara ni nani ?. Je ni yule aliyepewa kandarasi ya kujenga darasa kisha
akalijenga chini ya kiwango au ni wewe ambaye hukutaka kutoa ushirikiano kwa
vyombo husika hususani Takukuru.
Jamii nzima tunayo majukumu ya kuhakikisha
tunapambana na rushwa kwa njia yoyote ile. Njia ya kwanza ni kuhakikisha
hatupokei wala kutoa rushwa hii itasaidia sana katika kupunguza tatizo hili
hebu fikiria unataka huduma katika zahanati ya kijiji, mkeo anataka kujifungua
ni saa mbili za usiku muuguzi au mganga ameshalala lakini cha ajabu anakataa
kutoa huduma mpaka amepewe shilingi elfu 10 bila aibu unatoa pesa ile, mkeo
anajifungua halafu unashindwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama. Je,
itakuwaje kwa mtu ambaye hana hiyo elfu 10? kumbuka kuwa palipo na rushwa siku zote hakuna maendeleo.
Ndugu msomaji Rushwa ni mbaya iwe
kutoa ama kupokea kwa mtu mmoja mmoja na pia kwa jamii. Rushwa husababisha
maangamizi na hasara kwa umma, huharibu na kupoteza ndoto za maendeleo ya wanajamii,
Rushwa huleta udanganyifu na uongo
mahala pa uaminifu, dhuluma mahala pa haki, na hofu mahala pa amani na utulivu.
Palipo na rushwa siku zote hakuna
maendeleo mathalani
ajira zinajitokeza hususani za kwenda kujitolea JKT pale Kanembwa au
wanahitajika maafisa watendaji katika kata zetu labda za Kitahana , Kumsenga
ama Bunyambo ama katika mashirika binafsi kuna nafasi kama kumi (10) za kazi
kwa bahati mbaya bila kutoa kitu kidogo hata kwenye usaili huitwi. Sio watu
wote wenye uwezo wa kununua kazi, wakati mwingine mazingira yanatatanisha mno. Mathalani,
utakuta kijana ana vigezo vyote vya kazi, ila kwa vile hana uwezo wa kutoa kitu
kidogo, na kwa bahati mbaya masikini huyu hamjui mtu pale anapo omba ajira basi
hana chake tena, na kama tujuavyo sote kuwa rushwa ni adui wa haki, kwa hiyo
anakuwa amepoteza haki yake ya msingi na kwa bahati mbaya kijana huyu
anashindwa kutoa ushirikiano kwa maafisa wa TAKUKURU ili kushughulikia unyama
huo ili mwisho wa siku rushwa ikomeshwe kama sio kumalizwa kabisa.
Askari
wa usalama bara barani kila siku wanapokea rushwa kutoka kwa madereva boda boda
ama madereva wa magari ya abiria cha kushangaza hakuna hata anayetoa taarifa
ama kulalamika popote, matokeo yake kipato chake kisichozidi shilingi elfu 20
kila siku anakigawana na askari hao bila kujua kuwa anapoteza mapato ya
serikali ambayo yangeingia kama ushuru ama faini halali na baadae yangerudi na kuinufaisha jamii kwa
ujumla katika maswala ya bara bara , zahanati ama maji safi.
Ndugu
zangu nataka mjue kuwa aneyetoa na anayepokea rushwa wote wana makosa na
wanapaswa kuadhibiwa. Kila utakapoona dalili za rushwa ni vema ukatoa taarifa
kwa vyombo husika ili kuweka mazingira ya kumkamata mtuhumiwa na wewe kama Mtanzania
utakuwa umeonesha uzalendo wako kwa Taifa na kuokoa mali ambayo ingepotea bila
kufanya kazi yoyote ya maendeleo kwa Taifa lako.
Ndugu
msomaji lazima uchukue nafasi yako katika mambo ya nchi usimwachie tu mtendaji
ama mtumishi bila ushiriki wako. Hakuna kitakachowezekana bila ya kutimiza wajibu wako na kubaki tu kuwa
mtazamaji na mwisho wa siku utageuka kuwa mlalamikaji. Kama kiongozi wako wa
kijiji anapokea rushwa kwa nini ukae kimya usitoe taarifa kwa Takukuru? na
mwisho wa siku hatua ichukuliwe na maendeleo ya kijiji na jamii kwa ujumla
yaonekane.
Ni
wakati wa kila mwana Kibondo kwa imani yake kuwa na hofu ya Mungu kwa kuwa mtu anayemjua Mungu na mwenye hofu ya
Mungu hawezi kufanya mambo maovu ambayo yanamchukiza Mungu na yanaichukiza
jamii.
“Mcha
Mungu wa kweli atatenda haki; hawezi kumdhulumu binadamu mwenzake, hawezi kudai
rushwa ili atoe huduma kwa mtu, hawezi kuiba fedha za umma wala kujihusisha na ufisadi wa aina yoyote au uonevu wa aina
yoyote kwa maana anajua hayo yote ni dhambi mbele za Mungu
Nadhani
sasa ndugu msomaji utakuwa umeshaelewa ni kwa nini nimeanza na zile methali
pale mwanzo wa Makala hii na zaidi nilikuwa nalenga kuwa haiwezekani maafisa wa
TAKUKURU wakafanya kazi hii bila ushiriki wako kwa namna moja ama nyingine la
sivyo tutabaki kuwalaumu. Kama mzalendo ni lazima ushirikiane na maafisa hawa
katika kutokomeza rushwa miongoni mwa jamii. Pale unapohitajika basi utoe
ushirikiano bila kusita wengi wetu tunapoitwa mahakamani kwa ajili ya kutoa
ushahidi huwa tunakimbia hivyo kesi nyingi kuishia kufutwa mahakamani kwa
kukosa ushahidi na kusababisha kazi hii iwe ngumu kweli kweli kwa TAKUKURU na
mwisho wa siku jamii hupoteza kabisa Imani na chombo hiki chenye majukumu mazito
ya kuhakikisha rushwa inabaki kuwa historia hapa nchini. Ndugu msomaji kumbuka kuwa palipo na rushwa hakuna maendeleo siku zote hivyo unapaswa kushiriki kadri uwezavyo kama
mzalendo katika kuitokomeza.
Mwisho
kabisa ni vema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU)
iongeze juhudi za kuhakikisha wanatembelea vijiji vyote na kutoa elimu kwa
wananchi mara kwa mara ili kuwaelewesha wananchi namna ya kushiriki katika
mapambano haya ambayo mwisho wa siku kama elimu itaeleweka basi rushwa itakoma
au kupungua miongoni mwa jamii. Tukifanikiwa katika mapambano haya, rushwa ya
ngono, ajira kwa wasiositahili, ujenzi ya majengo ya umma chini ya kiwango na mengine mengi vitakoma kwa maendeleo ya
jamii na Taifa kwa ujumla. MWISHO 0786614043
No comments:
Post a Comment