Pages

Tuesday, February 25, 2014

maoni ya mwana kibondo aliyeko Russia kwa mbunge wa jimbo la muhambwe MH. Felix Mkosamali



KWAKO MBUNGE WANGU Felix Mkosamali Na WANANCHI WENZANGU WA KIBONDO SOMENI JAPO KIDOGO .
Niliposoma kwenye vyombo vya habari mwanzoni mwa mwaka 2010 na kuona umetangaza nia ya kugombea Ubunge ktk jimbo la Muhambwe nilifarijika sana na kuamini Wanamuhambwe tumepata mkombozi wa rasilimali zetu na mtetezi wa wanyonge tulioonewa toka kipindi cha ukoloni na hata nchi yetu ilipopata uhuru kamili.
Historia ya Kibondo(Muhambwe) inaniambia kwamba tulipata wabunge kama wawakilishi na watetezi wa wananchi wa Kibondo Bungeni kwa tiketi ya chama cha mapinduzi(CCM) kwa zaidi ya miaka 45 toka nchi yetu ipate uhuru. Nitaanza kumchambua mmoja mmoja kama ifuatavyo:
ARCADO DENIS NTAGAZWA.
Alikua Mbunge wetu zaidi ya miaka 15 ,lakini Kibondo haikuweza kupata barabara za uhakika ambazo zingekua chachu ya maendeleo ya kibondo kwa kuunganisha na mikoa ya jirani pia hata kutuunganisha na wilaya ya Kasulu.Kumbukumbu yangu inaniambia Kibondo tulikua na umeme wa jenereta miaka ya 80’s mpaka mwanzoni mwa 90’s ,lakini kutokana na usimamizi mbovu Kibondo tulirudi GIZANI na shuguli za uchumi zikazidi kuzorota,Genereta hizo zilizokua msitu wa Ushindo zilikufa na baadhi ya watu waliojiona wao ni wajanja waliiba vifaa mbalimbali vya jenereta hizo na miundombinu mingine ya umeme kama waya.Nilikua mdogo kipindi hicho lakini nachokumbuka baadhi yao hao waliohujumu hizo jenereta walikamatwa na kufikishwa mahakamani wakati huo Mzee wangu (Francis Mapigano) akiwa mkuu wa kituo cha polisi kibondo. Mwisho wa siku kibondo ilikosa umeme kabisa mbele ya macho ya Mzee Ntagazwa.
Nitakua simtendei haki Mzee Ntagazwa na mchoyo wa shukrani kwake nikisema ktk kipindi cha uongozi wake hakufanya kitu chochote cha maendeleo.Ninachokumbuka Mzee Ntagazwa ktk kipindi chake cha uongozi sekta ya elimu ilikua ipo juu ingawa Kibondo kulikua na shule chache za msingi,lakini zilikua zikifanya vizuri sana ukilinganisha na sasa,pia hata shule za sekondari zilikua zikifanya vizuri Kibondo sec(NENGO) na Mabamba Girls ingawa Malagarasi Sec ilikua haifanyi vizuri.
Miaka ya 2000 Kibondo upepo wa kisiasa ulibadilika na watu wengi walihitaji mabadiliko.Ndipo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Mh Felix Kijiko alipojitosa kwenye siasa za kibondo na kutokana na sera zake za kipindi hicho wanakibondo(Muhambwe) waliona ndio mbadala wa Mzee Ntagazwa.
FELIX KIJIKO.
Kutokana na uzoefu wake wa utumishi wa umma ,kweli wananchi walimchagua Mh Felix Kijiko kuwawakilisha wahambwe Bungeni.Katika kipindi chake cha miaka 5 Bungeni ,sijui wanakibondo tutamkumbuka kwa lipi? Mimi binafsi nitamkumbuka kwa RAMI chafu aliyoweka kibondo ,tena kwangu naona kama ni TUSI kubwa kwa wanakibondo kwa sababu rami ile ilijengwa kwa misingi ya kisiasa.Yani KIJIKO alijitaidi kuijenga harakaharaka tena chini ya kiwango kwasababu alitaka kututeka na kutupumbaza wanakibondo kifikira na tumwamini kua ametuletea maendeleo tena barabara ya rami kwa muda mfupi kuliko Mzee Ntagazwa alie kaa zaidi ya miaka 15 Bungeni.Target yake ilikua ni uchaguzi wa 2010,Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwafumbua na kuwaamsha wanakibondo na kuona nini Mh KIJIKO alitaka kuwapumbaza.Yawezekana yapo mazuri ambayo aliyafanya Mh Kijiko ndani ya miaka 5 ya uongozi wake bungeni,lakini mimi binafsi sikuyaona ,sijayaona na sitayaona.
FELIX MKOSAMALI.
Wanakibondo(Muhambwe) ambao sasa wanataka mabadiliko hawakuona ajabu wala gharama kuachana na chama kikongwe(CCM) na kuamua kukupa kura za ndio ndugu yangu,rafiki yangu Felix Mkosamali tena ukiwa bado ni mwanafunzi wa chuo kikuu (SAUT) kwa imani kuwa utaweza kututetea kwan bado ni kijana ambae unaweza kututumikia kwa muda mrefu tena bila kulala Bungeni kama wazee waliokutangulia.
Ni miaka miwili sasa toka wanamuhambwe tukuchague ingawa mimi binafsi sikupiga kura kutokana na umbali ila nilimwambia mama yangu na ndugu zangu kura ya ndio wakupe wewe sababu nilikuamini wewe kama kijana mwenzangu unaweza kusimamia haki za wanamuhambwe. Ajabu vijana ambao ndio walikua mstari wa mbele kuhakikisha unapata Ubunge 2010, leo hii ndio haohao ambao wanaonyesha kukosa imani na wewe na hii inatokana na wewe kushindwa kuonyesha mikakati ya kumkomboa mwanakibondo(muhambwe)katika Nyanja mbalimbali kama vile ajira , afya ,kilimo chenye tija, upatikanaji wa soko kwa wakulima ,michezo utamaduni n.k.Umeshindwa kusimamia uboreshwaji wa viwanja vya michezo kama vile mpira wa miguu,basketball netball na mpira wa wavu ambavyo vijana wengi hutumia kufanyia mazoezi, umeshindwa kuonyesha njia kwa wasanii wa kibondo kwa kusaidia kuibana halmashauri ijenge ukumbi mpya na wa kisasa wa burudani ili wasanii hao waweze kutumia kuonyesha sanaa zao pia na kuongeza kipato chao.
Naweza kusema ktk siasa za kibondo ndugu yangu umeanza vibaya na upepo unaweza kuwa mbaya zaidi kwako mwaka 2015.Muda bado unao wa kuweza kulekebisha pale ulipo anguka. Nakushauri ushirikiane na vijana wa kibondo hata KDF katika kuijenga Kibondo .Ni hatari sana kisiasa kukataliwa na rika lako(VIJANA)
Nikukumbushe kwamba endapo ndugu yangu Felix Mkosamali ukianguka kisiasa itakua ni anguko la Vijana wote wa kibondo na Tanzania kwa ujumla,Pia kumbuka wewe ndio mfano kwa vijana mblele ya wazee kama ukishindwa kuongoza basi ule usemi wa kijana hawezi kuongoza utakua umejidhihirisha na kibondo hatatokea kijana kuja kuaminiwa tena na wanakibondo.
Huu ni mtazamo wangu wa kisiasa juu ya kibondo (Muhambwe) ,Natanguliza samahani kwa yoyote Yule niliyomkwaza kwa namna moja ama nyingine.Pia nipo tayari kukosolewa kile nilichoandika kwa binadamu hatujakamilika.
ANGALIZO:
NIMESUKUMWA KUANDIKA HAYA IKIWA NI MOJA YA HARAKATI ZA KDF KUTAFUTA NAMNA YA KUMKOMBOA MWANANCHI WA KAWAIDA WA KIBONDO. NAOMBA ISTAFSIRIWE KAMA NI MOJA YA HARAKATI ZA KISIASA . MIMI KAMA MWANAKIBONDO NINA HAKI NA WAJIBU WA KUMKUMBUSHA KIONGOZI WANGU ATEKELEZE MAJUKUMU YAKE IPASAVYO ILI AWEZE KUTULETEA MAENDELEO.
WENU KATIKA UJENZI WA KIBONDO,
Nduhilubusa Mapigano. Moscow, Russia

No comments:

Post a Comment