Wito kwa mabloga wetu kuwa wabaunifu na kuacha kuibia kazi wenzao
Bila shaka wananchi wengi leo tumeshaanza kuzoea mablogu yaliyosambaa mitandaoni. Blogu zinatumika si tu kupokea habari haraka bali pia kumwezesha mtu yeyote mwenye tarakilishi (kompyuta) au simu kupeleka habari popote alipo.
Wimbi la “blogging” lilizaliwa kati ya 1995 hadi 1998 na kuanza kumea kwetu Tanzania kupitia mwanahabari Ndesanjo Macha miaka kumi iliyopita. Nakumbuka alivyokua akiniongelea juu ya fani hii kwa hamasa mwaka 2002. Baadaye kidogo aliendesha “Jikomboe Blog”, lililopambwa kwa taswira ya bonde lenye majani mabichi ya ukoka. Enzi hizo hakuchuma hata senti tano.
Ndesanjo alitabiri kwamba blogu ni dunia ya kesho ya mawasiliano. Na kweli leo kila mtu wakiwemo wafanyabiashara, wanafunzi, waalimu, wanataaluma, viongozi na wanasiasa hutumia mablogu kutuma na kupata habari.
Miaka hiyo kumi iliyopita vyombo vikubwa vya habari vya jadi (magazeti, redio na runinga) nchi zilizoendelea viliona umuhimu wake vikaanza kuunda blogu pembezoni mwa tovuti zake mama. Kwetu Tanzania vyombo vingi vya habari viliona blogu kama mshindani badala ya maendeleo.
Mambo yalianza kubadilika rasmi mwaka 2006 baada ya kifo cha wapenzi wawili wa Kitanzania waliouliwa kinyama Marekani. Blogu la Michuzi (ambalo halikua maarufu kama leo) na Radio Butiama ( huitwa “Podcast”) zilisimama dede kutangaza tukio hilo la kutisha. Hapo wengi ndipo tulipoanza kuona umuhimu wa bloga. Nilianza rasmi kublogu mwaka 2007. Nilichogundua siku za mwanzo ni kwamba Mabloga husaidiana sana. “Ukiwa mbinafsi huendelei kama Bloga” alisisitiza Ndesanjo.
Toka 2005 Ndesanjo, mtetezi wa mwanzo mwanzo wa blog za Kiswahili duniani, anafanya kazi shirika la “Global Voices.” Mtanzania huyu anaongoza kwa habari asilia za uchambuzi zaidi ya 4,220. Tofauti ya mtu kama Ndesanjo na mabloga wengi ni kuwa yeye ni mwanahabari hivyo huchanganya mitindo hii miwili kusanifu matukio. Si ajabu mwaka jana alishinda tuzo la Mwanablogu bora wa Kiafrika.
Lugha ya mabloga na vyombo asilia vya habari ni tofauti. Wanahabari wamesomea au kufanya mafunzo ya muda mrefu hivyo hufuata utaratibu wa lugha, masahihisho na uhariri mahsusi wa kazi zao. Bloga ni mtu yeyote tu anayetaka kuelezea jambo- si lazima awe amesomea uanahabari au kuyajua fika maadili na taratibu zake.
Leo mvua ya bloga Tanzania imegeuka bahari faraja. Mabloga ni wengi ; wanatupasha matukio kila sekunde! Wakati tukianza wanawake hawakua wengi. Mwaka jana mshindi wa Bloga bora Bongo alikuwa “Mwanamke na Nyumba.”
Zipo pia blogu ambazo zimegeuka makutano au kumbi za maoni na malumbano muhimu mathalan “Jamii Forums”, iliyoundwa 2006. Zipo zenye mafunzo ya mada kama “Al Hidaaya” inayofafanua Uislamu na Msahafu. Kuna zilizogeuka vijijarida au magazeti kama “Kwanza Jamii” la Maggid Mjengwa na “Tanzania Sports” lake Israel Saria kuhusu michezo toka London.
Mtanzania mkazi Denmark, Mikidadi wa “Global Tanzania Network” anauliza : “Suala lililopo ni vipi serikali hasa Wizara ya Habari itawaangalia na kuwalinda wana-bloga wetu au kuwasaidia kama nchi jirani za bara letu Afrika...mfano Kenya na Rwanda wanavyowasaidia mabloga wao?Tuwe wepesi kukubali wanabloga wanachangia saaana katika masuala mbalimbali ya uendelezaji wa mambo muhimu wa habari za ndani na za nje ulimwenguni.”
Blogu hizi vile vile zimegeuka ajira zinazowahudumia na kuwafariji wanahabari wake. Si kama enzi zile Ndesanjo akiendesha Jikomboe mwaka 2003! Blogu leo zimejazana matangazo ya biashara kiasi ambacho hata kuzifungua zinakera. Si tu nyanja za habari bali ni maduka. Ama kweli mtandao umekuwa biashara.
Ukweli ni huu. Watanzania tunakwenda na wakati. Mtandao ni uwanja wa fedha na vipato duniani!
No comments:
Post a Comment