Kwa kile kinachoaminika kuwa ni kukua kwa MGOGORO WA GESI Mkoani Mtwara na Kusini kwa ujumla, usiku wa kuamkia leo Mahakama ya Mwanzo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani imeteketezwa kwa moto huku nyumba ya Mbunge Hawa Gasia ikivunjwa vioo na kuchomwa motto wakati ile ya Mwenyekiti wa CCM Mtwara, ndugu Sinani ikiwa imevunjwa tu vioo.
Chanzo hasa cha vurugu hizo haziko wazi lakini wengi wanazihusisha na sakata la GESI kwani Hawa Gasia na Sinani wamekuwa kwa Muda Mrefu wakishutumiwa kwa kuchochea na kuridhia usafirishaji wa gesi hiyo kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam. Uchomaji huo wa moto uliambatana na vurugu na ulipuaji wa mabomu ya machozi kutoka kwa polisi na hadi wakafanikiwa kuzima jaribio la uchomaji wa Kituo cha Polisi cha Shangani.
Wakati huohuo kuna taarifa kutoka Masasi zikieleza nako kuibuka tukio la chomachoma mchana huu wa leo ikihusisha uchomwaji wa Offisi za Serikali, Polisi, nyumba za Wabunge na Offisi za CCM. Hali ya Masasi inaelezwa kuwa ni tete zaidi kuliko ilivyokuwa hapa Mtwara Mjini usiku wa jana ingawaje napo palikuwa na kimuhemuhe cha mabomu ya machozi kutoka kwa polisi.
Bado mpaka sasa haileweki ni nini hasa hatma ya mgogoro huu, maana kwa upande wake Serikali inaonekana kushikilia msimamo wake uleule wa kutaka kusafirisha gesi hiyo wakati upande wa raia wakiwa na msimao wao wa GESI KWANZA MAISHA BAADAYE, kwa maana kutoridhia usafirishaji wa gesi hiyo ikiwa ghafi kupelekwa Dar es salaam.
Wito wangu kwa Serikali ni kuwa, muda ni huu wa kukaa na wananchi ili kujadiliana juu ya mstakabali mzima wa tatizo hili na kutafuta suluhu. Muda ni huu kwa sababu si vyema kuacha hali iendelee kuharibika ndipo tuje baadaye tulazimike kuunda tume za watu kuchunguzwa. Si vibaya kwa Serikali kukiri au kurudi kwa raia na kusema pale ilipoteleza na kutafuta ni namna gani na ni njia ipi sahihi ya kuliendea suala hili.
Ewe Mungu! Ibariki Tanzania, Wabariki Watanzania.
No comments:
Post a Comment