MAENEO ya mikoa ya Morogoro, Mtwara na Dar es Salaam, jana
yaligeuka uwanja wa fujo na vurugu zilizosababisha vifo, majeruhi na
uharibifu wa mali, huku polisi wakitumia mabomu ya machozi kuwatawanya
wananchi.
Vurugu hizo zimehusisha wakulima na wafugaji wa
jamii ya Kimasai kwa upande mmoja wa Morogoro, Mtwara Mikindani wananchi
waliizingira nyumba ya Diwani wa Kata ya Mikindani kwa madai ya
kuwahifadhi watu wanaodaiwa kuwa washirikina ndani ya nyumba yake, huku
Dar es Salaam eneo la Kariakoo, polisi na Wamachinga wakipambamba na
Mgambo wa Jiji.
Mkoani Mororgoro mtu mmoja aliyefahamiwa kwa jina
la Mohamed Msigara (60) amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa
baada ya kutokea vurugu kati ya wakulima na wafugaji Kijiji cha Dumila,
wila yani Kilosa, baada ya wafugaji wa Jamii ya Kimasai kuingiza mifugo
yao kwenye mashamba ya wakulima yaliyo katika Kitongoji cha Mfulu,
Kilosa.
Pamoja na mauaji hayo, wasafiri waliokuwa
wakitumia Barabara ya Morogoro – Dodoma, nao walionja machungu ya vurugu
hizo, baada ya kukwama kwa saa 5 kutokana na wananchi wa kijiji hicho,
kufunga barabara kwa mawe, magogo ya miti na kuchoma magurudumu ya gari.
Wananchi hao walichukua hatua hiyo huku
wakisisitiza kutaka kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera,
ili kumaliza mvutano huo.
Katika vurugu hizo wanakijiji hao walivunja vioo
vya madirisha ya baadhi ya nyumba tano za kulala wageni, kuharibu gari
dogo aina ya Landcruser pamoja na kupora mali mbalimbali zi nazodaiwa
kumilikiwa na wafanyabiashara wa jamii ya Kimasai.
Kabla ya kufanya uharibifu huo saa 2:30 asubuhi,
wananchi hao walifanya maandamano sambamba na kusimama katikati ya
barabara, hali iliyosababisha polisi kufika eneo hilo kwa ajili ya
kuwadhibiti.
Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU), walifika eneo la
tukio 5:20 asubuhi na kufanikiwa kuwatawanya wananchi hao kwa kutumia
mabomu ya machozi, hatimaye kufungua barabara hiyo.
Pamoja na barabara hiyo ya Morogoro – Dodoma,
wananchi hao pia walifunga barabara ya Dumila- Kilosa, hivyo kuyafanya
magari yaliyokuwa yakitumia barabara hiyo kukwama kwa zaidi ya saa sita
na kusababisha usumbufu kwa wasafiri waliokuwa wakitumia barabara hiyo.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, wafugaji wa jamii
ya Kimasai wakiwamo wanawake na watoto walionekana kukimbilia kwenye
kituo kidogo cha Polisi Dumila kwa lengo la kujihami na kupata msaada wa
polisi kutokana na hofu ya kushambuliwa na wananchi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi
aliyekuwepo kwenye eneo la tukio, mkulima aliyefahamika kwa jina Mauya
Hamadi alisema kuwa wananchi wamelazimika kufanya vurugu hizo baada ya
wafugaji wa jamii ya Kimasai kuingiza mifugo kwenye mashamba ambayo
tayari yameshapandwa mazao na kufanya uharibifu.
Alisema kuwa tayari suala hilo walishalifikisha
kwa uongozi wa kijiji, kata, wilaya hadi mkoa, lakini hakuna jitihada
zozote zinazofanywa na viongozi, hivyo kulazimika kumtaka Mkuu wa Mkoa
Joel Bendera, kwenda kuzungumzia suala hilo, ambapo hata hivyo mkuu huyo
wa mkoa hakuwahi kufika eneo hilo hadi walipoamua kufanya maandamano
hayo.
No comments:
Post a Comment