Awali ya yote napenda kumshukuru mwenyezi Mungu mwingi
wa rehema , muumba mbingu na dunia kwa kuweza kunifikisha salama katika mwaka
huu wa 2014 nikiwa mwenye afya njema. Pia nichukue fursa hii kuwapa pole wote
walioanza mwaka huu wa 2014 wakiwa na matatizo mbali mbali kama magonjwa n.k. Pia wale wote waliotangulia mbele za
haki napenda kuchukua fursa hii kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma
aweze kuwasamehe madhambi yao na kuwalaza mahala pema peponi amina.
Ndugu zangu wanakibondo na kakonko, mimi kama
mzaliwa wa kibondo katika kijiji cha Mugunzu nina kila sababu za kuwapa salamu
zangu za mwaka mpya wa 2014 kwani ni mwaka ambao una maana sana kwetu wananchi
wa kibondo na kakonko. Nasema ni mwaka wenye maana sana kwetu kwasababu ni
mwaka ambao nchi yetu inategemea kuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa(
uchaguzi wa madiwani), hivyo ningependa kuzungumza nanyi japo kidogo na kutoa
mtizamo wangu katika Nyanja mbalimbali kama kisiasa,kijamii, afya elimu n.k.
1.UCHAGUZI
WA SERIKALI ZA MITAA.
Ndugu zangu kama awali nilivyosema nchi yetu
inategemea kuingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu wa 2014,
hivyo sisi kama wananchi wa kibondo na kakonko inabidi tuwe makini sana katika
uchaguzi wa madiwani ambao watakuwa makini katika kuzisimamia halmashauri zetu
za wilaya ya kibondo na kakonko.
Kwa nijuavyo mimi diwani ni muhimu sana zaidi ya
Mbunge lakini wengi wetu tunaamini kuwa Mbunge ndio ambaye anakazi kubwa ya
kuleta maendeleo ya jamii husika, sio kweli ndugu zangu, madiwani ndio wenye
umuhimu sana katika utendaji na usimamizi wa shughuli za maendeleo, kwani
madiwani ndio ambao tupo nao kila siku katika kata zetu na tunajumuika nao
katika shughuli mbalimbali za kila siku hata kero zetu wao wanazijua vizuri
kuliko wabunge kwasababu nao ni moja ya waathirika wa kero hizo. Hivyo basi
kutokana na dunia ya sasa kuwa imebadilika inabidi tuwe makini katika kuchagua
madiwani wenye uwezo na elimu nzuri ili waweze kutusaidia kuzisimamia
halmashauri zetu ambazo zimekua tatizo katika utendaji na usimamizi wa fedha za
miradi ya maendeleo. Vijana wenzangu ambao tumebalikiwa kupata elimu japo kidogo
tujitokeze kugombea hizi nafasi za udiwani kwani kuendelea kuwaachia watu wenye
elimu ya darasa la saba ni kuendelea kuiingiza jamii yetu katika lindi la
umasikini. Siwadhalau au kuwabeza watu wenye elimu ya darasa la saba, lahasha
ila naamini kuwa dunia ya leo ya sanyansi na teknolojia tunahitaji watu ambao
watakua na uwezo wa kupambanua mambo mbalimbali kwa undani zaidi na sio
ilimradi kukaa na kupokea posho za vikao.
Vijana wenzangu wengi wetu tunawaza sana UBUNGE na
kusahau UDIWANI ni wakati sasa wa kuugeukia udiwani ili tuweze kuwa na
Halmashauri zilizo bora na za mfano. Kwani tukiwa na Mabaraza ya MADIWANI
yaliyo na watu wenye elimu nzuri wataweza kuhoji na kusimami fedha za maendeleo
ya wilaya zetu ambazo watendaji wasio waaminifu wamekuwa wakizitafuna.
2.SIASA
ZA UDINI NA MAJI TAKA.
Ndugu zangu wanakibondo na Kakonko, tumesikia mengi
na kuona mengi katika uchaguzi mkuu uliopita wa 2010 na uchaguzi wa wawakilishi
katika mabalaza ya katiba 2013. Inaniuma sana na kusikitika sana kuona Kibondo
na sisi tumeanza kuingia katika siasa hizi za kidini, matusi na uzushi.
Kuendeleza siasa za namna hii ni kuiingiza jamii yetu katika migogoro mikubwa
na kupelekea chuki, uhasama . na uvunjivu wa amani katika wilaya zetu.
Tunajisahau kuwa hizi dini tumezipokea tu na hao waliotuletea hizi dini hata
wahazifuati kama sisi waafrika tunavyozifuata. Hivyo nachukua fursa hii
kuwaomba wanakibondo kutorudia kosa lile lililojitokeza katika uchaguzi wa 2010
na uchaguzi wa wawakilishi wa mabalaza ya katiba. Mimi binafsi siamini kama
kiongozi akitoka dini fulani ndio anaweza kuniondolea kero zinazonikabili
kuliko kiongozi aliyetoka dini nyingine, bali naamini kiongozi yoyote ambaye
anauwezo wa kiuongozi bila kuangalia dini yake ndio anaweza kunitatulia kero
zangu. Hivyo huu mtego wa udini inatupasa tuweze kuukwepa haraka sana na
atakayekua anafanya siasa za udini tumkanye mapema sana na tumnyime kura zetu
kwani huyo hatufai katika wilaya yetu na Taifa kwa ujumla.
Pia kibondo tumekuwa na siasa za chuki majungu na
fitna bila sababu yoyote, ni wakati wa kuacha hizi siasa ambazo matokeo yake ni
kuchukiana na mwisho wa siku kuuana. Wapo vijana wengi kibondo wanatumiwa na
wanasiasa bila wao kujua au wanajua na kupelekea kupandikiza chuki kwa vijana
wenzao. Inatupasa tutambue kuwa siasa sio uaduni hata pale tunapotofautiana
kimtizamo inabidi tuvumiliane. Na kutokana na hizo tofauti za kimtizamo na
kimawazo ndipo tunapopata mawazo mazuri ya kujenga na kutuletea maendeleo. Mtu
akipinga wazo lako sio kusema wewe ni mjinga au wazo lako ni la hovyo,
tukumbuke kwambia binadamu tunatofautiana sana kifikra.
3. ULIPUAJI WA MIRADI YA MAENDELEO.
a) .Mwaka jana nilikua Kibondo na kuona ile stendi
ya mabasi wenyewe tunaiita STENDI MPYA, ukweli nilitamani kulia kwani stendi
ile ni ya hovyo sana na sijui imegharamia shilingi ngapi. Stendi ile haina miundombinu kabisa ya maana
hata kituo cha polisi sina hakika kama kipo pale yani ipoipo tu , zaidi niliona
kokoto nyekundu ndo zilizo mwagwa pale. Ni wakati wa kusema hapana kwani
tunaibiwa mchana kweupe na sisi tunaona. Nilijiuliza maswali mengi sana ila
sikuweza kupata jibu mpaka leo sina jibu. Nashindwa kuamini kama baraza la
madiwani limekubaliana na ujenzi ule wa stendi ! Au mwezi wa 3 mwaka jana ndo
ilikua awamu ya kwanza ya ujenzi wa stendi ya wilaya ? sina jibu mpaka sasa
kwani nipo mbali. Ndugu zangu ndo maana nasema tuna kila sababu ya kuchagua
madiwani wenye elimu na uwezo wa kuhoji na kuisimamia halmashauri bila woga
kwani kwa mwendo huu kamwe hatuwezi kusonga mbele na kufikia ile nchi ya ahadi,
tutaendelea kuwa wilaya ya mwisho
kimaendeleo. Niwakati wa kuamka sasa na kusema hapana kwa watendaji wabovu wa
Halmashauri.
b). Ilikua mwaka jana nilisikia kwamba kiongozi wa
mbio za mwenge kitafa alizindua ujenzi wa uwanja wa mpira wa wilaya maarufu
kama uwanja wa Taifa,kinachonishangaza mpaka leo hii sijasikia taarifa kuwa
ujenzi umeshaanza zaidi naona picha kupitia facebook vijana wetu wakiendelea
kucheza kwenye uwanja uliojaa kokoto na mawe makubwa bila kuhofia kuumia
uwanjani. Kweli nimeamini sisi
watanzania tunaishi sana kwa mazoea. Haya yote yanatokea ikiwa madiwani
wapo na Mbunge, tena mbunge huyu ni kijana na yeye tumecheza wote kwenye uwanja
huo miaka ya 1999 na 2000 ikiwa kiwanja hicho kipo hivyohivyo. Tafadhari
wahusika simamieni pesa hizo za miradi ipasavyo.
4.FURSA ZA KIUCHUMI .
a).Kibondo ni moja ya wilaya ambazo zilitakiwa ziwe
zimepiga hatua kiuchumi kwa kuangalia geographic position. Kibondo tumepakana
na nchi ya burudi na tuna mpaka wa MABAMBA NA MUHANGE, tumeshindwa kutumia
fursa hii kibiashara , ni wakati sasa kwa wananchi wa kibondo kuamka na kuitumia hii fursa ya
mipaka kufanya biashara na nchi ya Burundi ili tujikomboe kiuchumi. Tufuate
taratibu za nchi zote mbili kisha tuanze biashara. Vijana wenzangu fursa ndio
hii, tuache kukaa vijiweni kuanzia asubuhi mpaka jioni tukipiga polojo
zisizokwisha kwani umri unasogea tunazeeka tupo vilevile. Bado vijana tumelala
sana, tuunde vikundi vya vijana kisha tuombe mikopo midogomidogo na tuanzishe
biashara. Tusiogope kukopa kwani hata hao matajiri wakubwa tunaowajua
ukiwafatilia wengi wana madeni, angalizo tu ni kwamba tunakopa pesa ili
tufanyie mambo ya kibiashara ila sio tukope pesa kisha tukeshe baa hapo mkopo
utauona mchungu. Serikali yenyewe inakopa iweje wewe uogope kukopa!! Amka
kijana wa kibondo na jitambue sasa.
b). Tumeshindwa kutumia ardhi yetu nzuri yenye
rutuba kwa kilimo chenye tija. Kibondo tumebarikiwa sana kuwa na ardhi yenye
rutuba , mito na mabonde mengi ambayo tukiyatumia vizuri tutaweza kunufaika
katika kilimo, niwakati sasa wa kuitumia ardhi yetu ambayo ni zawadi tuliyopewa
na Mwenyezi Mungu katika kufufua uchumi wetu. Wafanyabiashara wa kibondo
nawaomba mkigeukie kilimo kwani kupitia kilimo mtaweza kukuza uchumi wenu na
wilaya kwa ujumla pia mtasaidia kuzalisha ajira kwa vijana wengi wa kibondo
ambao wengi wanashinda vijiweni.
c). Madini ya chumvi na chokaa, kibondo pia
tumebahatika kupata madini ya chumvi na chokaa, ni wakati wa watendaji wa
serikali kuwahamasisha wafanyabiashara wakubwa wa Tanzania kuja kuwekeza
kibondo katika madini haya ili kuweza kuinua uchumi wa wilaya yetu, mwananchi wa
kawaida na Taifa kwa ujumla. Kutokana na kibondo kupakana na nchi ya Burundi
kama tutapata kiwanda cha chumvi na simenti wawekezaji wataweza kuuza nje ya
nchi kama Burundi, Kongo, Rwanda n.k. Pia wananchi wa kibondo wataweza kujenga
nyumba zilizo bora kwani gharama ya sementi itashuka kutokana na uzalishaji
kufanyika kibondo. Vilevile wilaya na mikoa ya jirani itaweza kunufaika na viwanda
hivi vitakavyojengwa.
5. UHARIBIFU WA MAZINGIRA, UHUJUMU WA MBOLEA ZA
RUZUKU NA WIMBI LA UJAMBAZI.
a). Toka wananchi wa kibondo wajikite katika kilimo
cha TUMBAKU kumekua na uharibifu mkubwa wa mazingira kwani uoto wa asili
umekuwa ukikatwa katika hatua za uandaaji wa mashamba ya tumbaku, misitu pia
imekua ikakatwa hovyo ili kupata kuni za kukaushia tumbaku hizo. Serikali
kupitia mamlaka husika inatakiwa kuweka sheria kali ili kuweza kuokoa mazingira
haya ambayo yanaharibiwa hovyo, pia serikali itoe elimu juu ya mazingira kwa
wananchi wanaojihusisha na kilimo hiki naikiwezekana itafute zao mbadala la
biashara ili kuokoa mazingira yetu.
b). Kitu ambacho kinaniuma sana ni kuona mbolea ya
ruzuku ikihujumiwa na wafanyabiashara mbalimbali wilayani Kibondo kwa kuwahonga
wananchi pesa kidogo na wananchi hao kuwauzia vocha za mbolea kwa bei ya chini
kisha wao kuwauzia tena mbolea hizo kwa bei ya juu. Mchezo huu mchafu umekua
ukifanywa na watendaji wa vijiji wasio waaminifu na waroho wa fedha kwa kuwakandamiza
wakulima kwakua wanajua kabisa wakulima wengi ni masikini na wanauelewa mdogo
juu ya vocha zinazotoka Serikalini. Hii hali niliiona ndani ya siku tatu
nilizokaa kibondo kipindi cha likizo na nilishindwa kuchukua hatua stahiki
kwakua nilikua na muda mchache. Sasa ni wakati wa kuwasema hadharani
wafanyabiashara hao na hao watendaji wa vijiji wasio waaminifu ili mkono wa sheria
uweze kuchukua nafasi yake. Wewe raia mwema na mpenda maendeleo ya kibondo toa
taarifa kwa njia ya siri kwenye vyombo vya ulinzi na usalama vya wilaya ili
kuweza kumsaidia huyu mkulima ambaye anadhurumiwa na hawa wafanyabiashara.
c). Tatizo la ujambazi bado lipo kibondo.Hili sitalizungumzia
sana kwakua sijalifanyia utafiti wa kutosha. Naimani operation kimbunga
imesaidia kupunguza ujambazi katika wilaya yetu. Kinachotakiwa ni sisi wananchi
wa kibondo kutoa taarifa polisi pale tu tunapomwona mtu ambaye hatumwelewi kwa
kufanya hivyo itatusaidia kupunguza au kutokomeza kabisa tatizo hili
linalotukabili si kibondo tu bali Taifa kwa ujumla.
Ndugu zangu yapo mengi ningependa nijumuike nanyi
katika mwaka huu mpya wa 2014 , lakini acha kwa leo niishie hapa na siku
nyingine nikipata nafasi nijaongea mengine kwa ajiri ya maendeleo ya KIBONDO.
Nawatakia afya njema, mafanikio ya kiuchumi katika
mwaka huu wa 2014 na Mungu awafanikishie kila lile jema mlilopanga kufanya
katika mwaka huu.
HIZI NDIZO SALAMU ZANGU ZA MWAKA MPYA WA 2014 KWENU
WANAKIBONDO WENZANGU.
NI MIMI NDUGU YENU,KIJANA MWENZENU NA MTOTO WENU.
NDUHILUBUSA
MAPIGANO
MOSCOW,
RUSSIA
2014.
ASANTENI
SANA.
No comments:
Post a Comment